THE
SEVENTH-DAY ADVENTIST CHURCH
MARA
CONFERENCE
AGAPE GOSPEL SINGERS-MUSOMA 2013
KATIBA
TOLEO I
[Katiba
hii imeandaliwa ili kulinda mfumo mzima wa kiutendaji wa kikundi]
SEHEMU YA I
KUHUSU
KIKUNDI
- JINA
Jina rasmi la Kikundi litakuwa Agape Gospel Singers (AGS) 2013. Jina
hili litatumika katika shughuli zote rasmi za kikundi, kanisa, mialiko na katika
matangazo mbalimbali.
- ANUANI
Kikundi
kitakuwa na Ofisi katika Manispaa ya Musoma-Mtaa wa Kamnyonge. Anuani
itakakuwa:
Agape Gospel Singers,
S.L.P
301
MUSOMA.
Barua pepe: agsmusoma2013@gmail.com
Tovuti/Blog: AGAPE
GOSPEL SINGERS-MUSOMA
- MOTO
PIGA MBIU TANGAZA MAREJEO YA YESU KRISTO
ULIMWENGUNI KOTE
- MAONO
Kwaya ya AGS inalenga kutoa fursa za kujifunza na
kutoa huduma ya neno la Mungu kwa kuburudisha na kuelimisha kupitia nyimbo za
ibada na matamasha. Ili kujitangaza na kujitanua ndani na nje ya mipaka ya Mara
Conference na Union, wanakikundi watatazamiwa kutimiza wajibu wao wa kuhubiri
kupitia muziki na kutenda kama mabalozi wema wa Yesu Kristo ndani na nje ya
kanisa.
- MWONGOZO
Kikundi kimedhamiria kuwasaidia
wanakwaya kujifunza muziki wa injili ili kuwawezesha kuwa waimbaji wa viwango
vya juu, kuwa wataalam wenye ujuzi wa kufundisha muziki, waweze kujiajiri
kupitia muziki na hivyo kusaidia maendeleo ya kanisa na ya jamii.
SEHEMU
YA II
IMANI
YA KIKUNDI
- MISINGI YA IMANI
Misingi
ya Imani ya kikundi inajibainisha katika mambo yafuatayo:
Tunaamini
katika:
1.
Nguvu na uweza wa Bwana wetu Yesu Kristo.
2.
Upekee, ukamilifu, ukweli na mamlaka ya Biblia
Takatifu.
3.
Ulazima na uwezo wa ufufuo wa matumaini mapya
unaotokana na kifo cha Yesu Kristo msalabani kwa ajili ya kuuokoa ulimwengu.
4.
Uwepo wa nguvu ya Roho Mtakatifu kwa kazi ya
matengenezo na uumbaji mpya.
5.
Matumaini ya kurudi kwa Bwana wetu Yesu Kristo
kwa ajili ya ufufuo na uzima wa milele.
6.
Uwezo na karama ya uimbaji kutoka kwa Mungu Baba
kwa ajili ya kueneza injili ya Bwana wetu Yesu Kristo.
- MATARAJIO
Kikundi
kina matarajio makubwa kwamba, kwa umuhimu wa kipekee, viongozi wote wa
kuchaguliwa na kuteuliwa wa kikundi, wanachama na vikundi, watu binafsi au
makampuni watakaoalikwa kwa ajili ya kuchangia kama njia ya kutimiza maono ya
kikundi, bila ya kufungwa na misingi ya imani hapo juu, watajitoa kwa moyo kwa
kadri Mungu alivyowajalia.
SEHEMU
YA III
MALENGO
YA KIKUNDI
- MALENGO YA MSINGI
1.
Kushuhudia kwamba Yesu Kristo ni Mungu halisi, na
kujifunza kuwaongoza wengine kuamini kuwa Yesu ni Bwana na Mwokozi wetu. Lengo
hili linatimizwa kupitia nyimbo na mawasiliano.
2.
Kuwasaidia wakristo kukua katika imani kama
wanafunzi wa Yesu na kuwafundisha kuliona kanisa kuwa ni nyumbani kwao, kwa
kusoma na kujifunza Biblia, kwa maombi na ushirika wa Yesu Kristo.
3.
Kuonyesha mwito wa Mungu kwa wanadamu kupitia
maono ya kanisa.
- MALENGO YA ZIADA
1.
Kuhamasisha juu ya maendeleo ya elimu ya kiroho
na mafunzo ya fani ya muziki.
2.
Kufanya mahubiri ya hadhara ili kuongoa roho
nyingi kupitia nyimbo.
3.
Kuwatia moyo waliokata tamaa ya maisha kupitia
nyimbo za injili ya Yesu Kristo.
4.
Kutumia mapato ya kikundi kufungua miradi
mbalibali ili kutoa ajira kama sehemu ya mkakati wa kuvuta na kuwaleta
kanisani.
- MAHITAJI
1.
Vifaa toshelevu vya kisasa vya muziki
vinavyokidhi mahitaji ya kwaya.
2.
Usafiri wa kwaya.
3.
Jengo la ofisi ya kikundi.
SEHEMU YA IV
UANACHAMA NA USHIRIKA
Uanachama wa AGS upo wazi kwa
jamii ya washirika wa kanisa la Wa-adventista wa Kisabato wa makanisa yaliyopo
ndani ya Manispaa ya Musoma. Mwanachama atakuwa yule atakayeafikiana na matakwa
ya sehemu ya II A na B ya katiba hii. Mwanachama atakuwa yule aliyejaza fomu ya
maombi ya uanachama na kuthibitishwa au kupitishwa na bodi ya wakurugenzi ya
kikundi kwa kukidhi vigezo vyote vitakavyopangwa na mkutano mkuu wa kikundi.
- AINA ZA UANACHAMA.
1. WANACHAMA WAANZILISHI
Hawa ni
wanachama waliobuni wazo na kuamua kuanzisha kikundi. Ni waanzilishi walioweka
misingi, taratibu na kuandaa mipango yote ya kikundi.
2. WANACHAMA WAPYA
Hawa ni
wanachama walioomba na kukubaliwa kujiunga na kikundi baada ya kufuata taratibu
na kutimiza vigezo vyote vya uanachama kwa mujibu wa katiba.
3. WANACHAMA WATEULIWA
Hawa ni
wanachama waliopendekezwa kutokana na fursa zao kwa ajili ya kukisaidia
kikundi. Wamepewa uanachama kutokana na taaluma na au ujuzi walionao.
- SIFA, HAKI NA WAJIBU WA MWANACHAMA
1. SIFA
i.
Mwanachama wa kikundi atakuwa M-Adventista
M-Sabato mwenye ushirika katika kanisa lake anakosali.
ii.
Awe na akili timamu na awe na umri kuanzia miaka
18 na kuendelea.
iii.
Ajue kusoma na kuandika.
2. HAKI
i.
Kila mwanachama atakuwa huru kutoa mawazo yake
sahihi ndani ya kikundi
ii.
Kila mwanachama atakuwa na haki ya kusikilizwa na
kusikiliza mawazo ya wenzake kwa upendo na unyenyekevu.
iii.
Kila mwanachama atakuwa na haki ya kuchagua au
kuchaguliwa kuwa kiongozi wa kikundi.
iv.
Ni haki ya mwanachama kutoa taarifa sahihi kwa
mtu sahihi na kwa wakati sahihi juu ya matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu
wa raslimali ya kikundi na matendo yote yasiyomtukuza Mungu miongoni mwa
wanakikundi.
v.
Ni haki ya mwanachama kuhudhuria matamasha ya
injili na mialiko mbalimbali inayohusiana na shughuli za kikundi.
3. WAJIBU
i.
Kila mwanachama ana wajibu wa kuhudhuruia vikao
na mikutano inayomhusu kwa nafasi yake katika kikundi.
ii.
Ni wajibu kwa kila mwanachama kufika kwa wakati
na kushiriki kwa ukamilifu mazoezi yote ya kwaya.
iii.
Ni wajibu wa mwanachama-mwanakwaya kuwa na sare
zote za kwaya zinazotakiwa kwa wakati na katika mazingira muafaka.
iv.
Kila mwanachama anawajibika kutekeleza kwa
ufanisi na kwa wakati majukumu yake yote atakayopangiwa na kikundi.
v.
Ni wajibu wa kila mwanachama kulipa kiingilio,
ada na michango yote stahiki kwa kadri
itakavyokuwa inaamriwa na vikao halali vya kikundi.
SEHEMU
YA V
UONGOZI
NA MAJUKUMU
- MKURUGENZI MKUU
1.
Atakuwa
kiongozi mkuu wa kikundi.
2.
Atasimamia
shughuli zote za AGS ikiwa ni pamoja na masuala ya imani, utawala, mipango,
vikao, uchumi, mahusiano na mawasiliano, matangazo, raslimali, na usimamizi
watovuti ya kwaya.
3.
Atawapangia
majukumu viongozi na wanachama wengine na atakuwa kiungo muhimu kati ya
wanakwaya na viongozi wa kikundi.
4.
Atahudumu
kama mwenyekiti wa vikao vyote vya bodi ya wakurugenzi na mkutano mkuu wa
kikundi.
5.
Ataratibu
na kusimamia mialiko na safari zote za kikundi ndani na nje ya Manispaa ya
Musoma.
6.
Atashauriana
na bodi ya wakurugenzi kufanya uteuzi wa wataalamu muhimu wanaohitajika
kuimarisha shughuli za kikundi.
- KAIMU MKURUGENZI MKUU
1.
Atasaidia
na kusimama kwa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu pale asipokuwepo
2.
Atahudumu
kama msimamizi mkuu wa shughuli zote za matangazo na machapisho kwenye
majarida, mitandao, vipeperushi n.k.
3.
Atahusika
na ubunifu, uandaaji na ugawaji wa sare za kwaya.
4.
Atawajibika
kwa majukumu mengine kwa kadri atakavyopangiwa na Mkurugenzi Mkuu.
- KATIBU MTENDAJI
1.
Atawajibika
kuchukua na kuandaa taarifa ya mahudhurio ya vikao, mazoezi ya kwaya na matukio
mengine ya wanachama.
2.
Ataandaa
na kutunza taarifa na mihtasari yote ya vikao vyote vya bodi ya wakurugenzi na
mkutano mkuu.
3.
Ataandaa
ripoti zote za kikundi zinazotarajiwa kutumwa au kusambazwa kwa taasisi, watu
binafsi au makampuni yenye mahusiano na kikundi.
4.
Atawajibika
kwa majukumu mengine atakayopangiwa na Mkurugenzi Mkuu. Iwapo atapata udhuru wa
mahudhurio ya kikao, nafasi yake itakahimiwa na mwanachama yeyote miongoni mwa
wajumbe wa bodi ya wakurugenzi.
- MKURUGENZI WA UCHUMI NA FEDHA
1.
Ataandaa
bajeti ya mwaka ya kikundi kwa kushirikiana na bodi ya wakurugenzi.
2.
Atawajibika
kuandaa na kutolea taarifa kwa wakati matumizi yote ya fedha yaliyopangwa
kutumiwa na kwaya katika shughuli zake za kila siku.
3.
Atapokea
na kuhakikisha anatunza kwa usahihi mapato yote yatokanayo na michango na
makusanyo yote ya kikundi kutoka vyanzo mbalimbali.
4.
Atawajibika
kwa majukumu mengine ya kikundi kwa kadri atakavyopangiwa na Mkurugenzi Mkuu.
- MKURUGENZI WA MAKTABA NA MAWASILIANO
1.
Atakuwa
mwangalizi na msimamizi mkuu wa maktaba ya kwaya.
2.
Ataandaa
na kutunza vifaa vyote vya muziki na mafaili yote (Kanda na CD’s).
3.
Atatunza
na kuifanyia marekesho tovuti ya kikundi na kuhakikisha pia anaiwekea taarifa
zote stahiki. Atakuwa chini ya uratibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu.
4.
Ataandaa
na kutunza taarifa zote za machapisho, picha na sare zote za kwaya.
5.
Atapokea
na kutoa taarifa zote ndani na nje ya kikundi.
6.
Atawajibika
kwa majukumu mengine ya kikundi kama atakavyopangiwa na Mkurugenzi Mkuu.
- MKURUGENZI WA MUZIKI NA MAHUSIANO
1.
Atashirikiana
na wasaidizi wake kuongoza kwaya katika shughuli zote zinazohusu muziki na
kufanya uteuzi wa nyimbo kwa ajili ya Ibada na matamasha ya injili.
2.
Atashirikiana
na wataalamu wa ndani na nje ya kikundi kutunga na kufundisha nyimbo katika
kwaya na kuratibu matumizi ya majukwaa na kurekodi nyimbo.
3.
Yeye na
wasaidizi wake watatoa ushauri na mapendekezo juu ya muundo wa kwaya na kuwa kiungo
muhimu kati ya mwanakwaya mmoja mmoja na kikundi.
4.
Atasikiliza
na kutolea ushauri shida na matatizo mbalimbali ya wanakwaya.
5.
Atawajibika
kwa majukumu mengine atakayopangiwa na Mkurugenzi Mkuu. Bodi ya wakurugenzi
itateua mkurugenzi mpya kuchukua nafasi wazi itakayoachwa na mkurugenzi wa
kwaya kwa sababu yoyote ile.
SEHEMU YA VI
VIKAO NA MAJUKUMU
Kikundi
kitaendesha shughuli zake kwa mujibu wa vikao halali vya wanachama. Kutakuwa na
vikao vya aina kuu tatu: Mkutano mkuu, Bodi ya wakurugenzi na Baraza la wadhamini. Kila mwanachama anatarajiwa
kuhudhuria vikao vyote vinavyomhusu kwa mujibu wa katiba. Mwanachama
atakayekosa vikao vitatu (3) na ama mazoezi ya kwaya mfululizo pasipo taarifa rasmi atachukuliwa hatua ya kinidhamu
kwa kadri itakavyoamriwa na bodi ya wakurugenzi.
- MKUTANO MKUU
1.
Mkutano
mkuu ndicho kikao kikuu cha wanachama wote.
2.
Mkutano
mkuu utafanyika mara mbili (2) kwa mwaka. Theluthi mbili ya wajumbe inaruhusu
kufanyika kwa mkutano.
3.
Mkurugenzi
Mkuu ndiye atakuwa mwenyekiti wa kikao
MAJUKUMU YA MKUTANO MKUU
a.
Mkutano
mkuu ni kikao chenye maamuzi ya mwisho kwa shughuli zote za kikundi.
b.
Kitakuwa
ndicho kikao cha kuchagua viongozi wa kikundi na kuidhinisha Bodi ya wadhamini.
c.
Mkutano
mkuu utapitisha bajeti ya kikundi na una mamlaka ya kufanya marekebisho ya
viwango vya michango ya kikundi.
d.
Kikao
kitapokea na kujadili taarifa ya mapato na matumizi kutoka bodi ya wakurugenzi.
e.
Mkutano
mkuu ndicho kikao chenye mamlaka ya kurekebisha au kubadili katiba kwa kadri itakavyofaa kulingana na mahitaji ya
kikudi ya wakati huo.
f.
Mkutano
mkuu ni kikao kinachotengeneza sera, taratibu na miongozo ya uendeshaji wa
kikundi na kutoa maagizo kwa bodi ya wakurugenzi kwa ajili ya utekelezaji.
- BODI YA WAKURUGENZI
1.
Bodi ya
Wakurugenzi ni kikao kitakachoundwa na wakurugenzi wote sita (6) wa kikundi
pamoja na wajumbe wawili watakaochaguliwa na mkutano mkuu.
2.
Kikao
kitafanyika mara moja kila baada ya miezi miwili (2). Theluthi mbili ya wajumbe
itaruhusu kufanyika kwa kikao.
3.
Mkurugenzi
Mkuu ndiye atakuwa mwenyekiti wa kikao.
MAJUKUMU
YA BODI YA WAKURUGENZI
a.
Bodi ya
Wakurugenzi ni kikao kitakachosimamia na kuratibu shughuli zote za kila siku za
kikundi. Itasimamia utekelezaji wa maagizo yote ya mkutano mkuu
b.
Kikao
kitapokea na kujadili taarifa ya mapato na matumizi ya fedha za kikundi na
kuwasilisha taarifa hiyo katika mkutano mkuu.
c.
Bodi
itaratibu shughuli zote za uchaguzi za kikundi ikiwa ni pamoja na kuteua Bodi
ya wadhamini na wasaidizi wa mkurugenzi wa muziki.
d.
Kikao
kitakuwa na majukumu ya kuidhinisha matumizi yo yote ya fedha ndani ya kikundi.
e.
Bodi
itapokea, itajadili na kuratibu mabadiliko ya katiba na kupitisha maombi ya
wanachama wapya.
f.
Bodi ya
Wakurugenzi ina wajibu wa kupokea na kujadili taarifa ya tabia na mienendo
isiyo ya kumtukuza Mungu itakayofanywa na viongozi au wanachama kabla ya
kufikisha mapendekezo ya taarifa hiyo katika mkutano mkuu kwa ajili ya maamuzi.
- BARAZA LA WADHAMINI
1.
Baraza la wadhamini itaundwa na wajumbe watatu
watakaoteuliwa na Bodi ya wakurugenzi. Mkurugenzi mkuu atakuwa mjumbe mwalikwa.
2.
Baraza
itafanya kikao kimoja kila mwaka. Mwenyekiti wa kikao atachaguliwa miongoni mwa
wajumbe.
MAJUKUMU
YA BODI YA WADHAMINI
a.
Kusimamia
misingi yote ya kanisa na kikundi na kuhakikisha kuwa inafuatwa
b.
Kudhamini
shughuli zote za kikundi ikiwa ni pamoja na ziara na mialiko, pia kushiriki
kukitafutia kikundi ufadhili.
SEHEMU
YA VII
UCHAGUZI
Mkutano mkuu wa uchaguzi utafanyika kila baada ya miaka
mitatu (3). Uchaguzi wa dharura unaweza kuitishwa muda wowote ili kuziba nafasi
inayoweza kuachwa wazi kutokana na ukomo wa uongozi kama inavyofafanuliwa
katika sehemu ya VIII ya katiba hii. Shughuli za uchaguzi ndani ya kikundi
zitazingatia utaratibu ufuatao:
- Bodi ya Wakurugenzi itakuwa na mamlaka ya kufanya uteuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ambaye kwa mujibu wa matakwa ya katiba hii atatoka nje ya kikundi. Huyu aweza kuwa mzee wa kanisa, mchungaji wa ngazi ya mtaani au Conference kwa kadri ambavyo bodi itaona anafaa.
- Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi atapendekeza majina mawili (2) ya wajumbe wa Tume yake ambao waweza kutoka ndani au nje ya kikundi ambao si miongoni mwa viongozi wanaomaliza muda wao. Majina hayo yatawasilishwa kwenye kikao cha Bodi ya Wakurugenzi kwa ajili ya uthibitisho.
- Tume ya uchaguzi itaundwa mwezi mmoja kabla ya siku ya uchaguzi..
- Wanachama watakaoomba kuchaguliwa watapaswa kujaza fomu maalumu za maombi zitakazoandaliwa na Tume ya Uchaguzi. Fomu zitaonyesha nafasi ya uongozi.
- Viongozi waliomaliza muda wao wanaruhusiwa kujaza fomu za maombi. Hakuna kipindi maalumu cha ukomo wa uongozi hadi katiba hii itakapofanyiwa marekebisho.
- Nafasi za uchaguzi ni:
a.
Mkurugenzi Mkuu
b.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu
c.
Katibu Mtendaji
d.
Mkurugenzi wa Fedha
e.
Mkurugenzi wa Maktaba na Mawasiliano
Nafasi ya Mkurugenzi wa Kwaya
na Mahusiano ni ya kitaaluma. Mkurugenzi atateuliwa na Bodi ya Wakurugenzi.
- Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi atapanga tarehe na muda wa kufanya uchaguzi. Atapanga utaratibu ufuatao ili kurahisisha zoezi zima la uchaguzi:
a.
Wagombea wote lazima watajwe kwa nafasi
wanazogombea. Kila mgombea atapewa fursa ya kujitambulisha na kueleza kwa nini anafaa
kuchaguliwa kwa nafasi anayoiomba.
b.
Utaratibu wa uchaguzi ni wa kura ya
siri na Mwenyekiti atazingatia mpango maalumu kama ilivyoonyeshwa katika
kipengele nambari 6 hapo juu.
c.
Nafasi yenye mgombea mmoja,
Mwenyekiti wa Tume atamtangaza kuwa mshindi moja kwa moja baada ya kupigiwa
kura ya NDIYO.
d.
Kwa nafasi yenye wagombea zaidi ya
mmoja, mshindi atapatikana kwa wingi wa kura zaidi ya wagombea wenzake.
- Kadri ya 75% ya mahudhurio ya wanachama itaruhusu kufanyika uchaguzi.
- Matokeo ya uchaguzi yatatangazwa na Mwenyekiti wa Tume na ndiyo yatakuwa matokeo ya mwisho.
SEHEMU
YA VIII
UKOMO
WA UONGOZI NA UANACHAMA
Tunalenga kuhakikisha kwamba kila kiongozi na mwanachama anajiimarisha
na kusimama katika misingi ya imani na kutimiza malengo yote ya kikundi kama
ilivyoelezwa katika sehemu ya II na III ya katiba hii. Kushindwa kukidhi
matakwa ya misingi na malengo ya kikundi kutasababisha ukomo wa uongozi au
uanachama kama inavyofafanuliwa hapa chini:
- UKOMO WA UONGOZI
1.
Kipindi cha uongozi ni miaka mitatu.
Endapo kiongozi hatochaguliwa tena kurudia madaraka yake uongozi wake utakuwa
umekoma.
2.
Ukomo wa uongozi utafika endapo
kiongozi aliyepo madarakani atajiuzulu kwa ridhaa yake, kufutwa uanachama au kusimamishwa
uongozi kwa manufaa ya kikundi.
3.
Ukomo wa uongozi utafika endapo
kiongozi aliyeko madarakani atahama au kuaga dunia (kifo).
- UKOMO WA UANACHAMA
1.
Ukomo wa uanachama utafika endapo
mwanachama atajiuzulu uanachama kwa ridhaa yake au kuachishwa uananchama kwa
makosa yake.
2.
Uanachama utakoma endapo mwanachama
atashindwa kulipa ada na michango mingine iliyoamriwa na kikundi kwa vipindi
vitatu mfululizo.
3.
Kifo, uhamisho na kushindwa
kuhudhuria vikao mara tatu mfululizo ni miongoni mwa vigezo vinavyotumika
katika ukomo wa uanachama.
SEHEMU
YA IX
MAPATO
YA KIKUNDI
Kikundi
kinatarajia kukusanya mapato yake kutoka vyanzo mabalimbali kama
ilivyoorodheshwa hapa chini:
- Fedha za kiingilio (Tshs. 5,000/=) na Ada za uanachama kwa mwaka (Tshs. 10,000/=)
- Michango mbalimbali ya wanachama.
- Michango ya wahisani na wadau mbalimbali.
- Harambee na uzinduzi wa albamu za kwaya.
- Mauzo ya kanda na CD’s.
- Mikopo toka taasisi mbalimbali za fedha.
- Miradi itakayoanzishwa na kikundi.
Kikundi
kina maono ya kutumia makusanyo yake katika mambo yafuatayo:
- Kulipa Zaka na Sadaka.
- Kuchangia katika shughuli za maendeleo ya kanisa k.v. huduma za injili, afya, elimu na ujenzi.
- Kutoa huduma ya msaada kwa watu wenye uhitaji walio ndani na nje ya kanisa.
- Kuhudumia na kuendesha shughuli mbalimbali za kikundi.
- Kutoa msaada wa kimahitaji kwa matatizo yatakayowakabili wanachama.
NYONGEZA:
- Kikundi kitafungua na kumiliki Akaunti katika Benki ya CRDB tawi la Musoma.
- Katiba inatambua watia sahihi watatu (3) kwa nyadhifa zao kama ifuatavyo:
a.
Katibu Mtendaji…………………………………Mtia
sahihi mkuu.
b.
Mkurugenzi wa Fedha
c.
Mjumbe mmoja toka Bodi ya
Wakurugenzi.
- Wajumbe wawili kati ya hao watatu, Sahihi ya Katibu Mtendaji ikiwa ya lazima, wanaruhusiwa kutoa pesa Benki.
SEHEMU
YA X
MAREKEBISHO
YA KATIBA
- Katiba hii imeandaliwa kwa kusudio la kukidhi haja na mahitaji ya kikudi. Iwapo itashindwa kufikia malengo hayo kwa kipindi au mazingira muafaka, Bodi ya Wakurugenzi itawajibika kuifanyia marekebisho kabla ya kuifikisha Mkutano Mkuu kwa maamuzi ya mwisho.
- Mwanchama yeyote aweza kuleta hoja ya mabadiliko mbele ya Bodi ya Wakurugenzi kwa ajili kupitia na kufanyia marekebisho.
- Siku ya tukio la marekebisho, kwaya itapendekeza mwakilishi mmoja atakayeungana na Bodi katika kikao husika. Marekebisho yaweza kufanywa kwa njia ya kura pale muafaka unaposhindwa kufikiwa.
- Marekebisho ya katiba hayatokuwa halali hadi nakala ya marekebisho hayo itakapopitishwa na 75% ya kura za mkutano mkuu chini ya ushauri wa Mwanasheria atakayependekezwa na Bodi ya Wakurugenzi.
- Marekebisho ya katiba yatafanyika mara moja katika kipindi cha miaka mitatu au pale ambapo itapoonekana inafaa kulingana na mahitaji ya kikundi.
ANDIKO HILI
LIMEANDALIWA NA KUIDHINISHWA LEO JUMAMOSI, TAREHE 20 JULAI, 2013
BODI YA WAKURUGENZI:
Na.
|
Jina
|
Sahihi
|
Cheo
|
1
|
Mkama L. Rugina
|
Mkurugenzi Mkuu
|
|
2
|
Fredy N. Jeje
|
Kaimu Mkurugenzi
Mkuu
|
|
3
|
Emmy Msiba
|
Katibu Mtendaji
|
|
4
|
Bethy Msiba
|
Mkurugenzi wa Uchumi
na Fedha
|
|
5
|
Gaya Masatu
|
Mkurugenzi wa
Maktaba na Mawasiliano
|
|
6
|
Akiba Mashenene
|
Mkurugenzi wa
Muziki na Mahusiano
|
|
7
|
Phoebe Yonah
|
Mjumbe
|
|
8
|
David Mayunga
|
Mjumbe
|
1 comment:
Kazi nzuri, hongereni sana
Post a Comment